KULEA VIFARANGA ULISHAJI VIFARANGA/CHANJO/DAWA.

UFUGAJI BORA WA NG'OMBE WA ASILI

Ng’ombe ni mnyama jamii ya nyati ambaye hufugwa na mwanadamu. Nchini Tanzania ng’ombe ni mnyama mkubwa kuliko wanyama wengine wote wanaofugwa vijijini.Ng’ombe huwapatia wanadamu nyama, maziwa, ngozi na mbolea.

Ng’ombe hufugwa katika mikoa yote ya Tanzania.

2.0 AINA YA NG'OMBE WAFUGWAO TANZANIA.

2.1.0 Ng’ombe wa asili

i. Zebu

ii. Ankole

iii. Boran

2.2.1 Ng’ombe wa Kigeni/Kisasa

i. Friesian

ii. Ayrshire

iii. Guensey

iv. Jersey

v. Brown Swiss

vi. Sahiwal

2.2.2 Ng’ombe Chotara

Ng’ombe chotara ni wale waliopatikana kutokana na kuchanganya damu za aina mbili au zaidi za ng’ombe wa kigeni na wa asili. Ng’ombe chotara wana sifa bora mchanganyiko za ng’ombe wa kigeni na asili. Mpwapwa; wamezalishwa kutokana na ng’ombe aina ya Boran, zebu, sahiwal na ng’ombe kutoka Ulaya.

3.0 SIFA ZA NG'OMBE WA ASILI.

i. Wana uwezo wa kustahimili magonjwa

ii. Hustahimili muda mrefu bila malisho yakutosha

iii. Wanaweza kutembea mwendo mrefu kutafuta maji na malisho

iv. Nyama na maziwa yao yana ladha nzuri

v. Maziwa yao yana mafuta mengi kuliko ya ng’ombe wa kisasa

3.1.0 Mapungufu ya ng’ombe wa asili

i. Wana umbile dogo

ii. Huchukua muda mrefu kuzaa (Ndama moja kila baada ya miaka mwili)

iii. Hutoa maziwa kidogo

4.0 KOO ZA NG'OMBE WA ASILI NA SIFA ZAO.

4.1.0 Zebu

i. Wana nundu

ii. Wana pembe fupi

iii. Wana umbo dogo

iv. Wana rangi nyingi tofauti tofauti katika sehemu mbalimabali

v. Wanapatikana katika mikoa yote ya Tanzania

4.2.0 Ankole

i. Ng’ombe jike hawana nundu ila madume wana nundu ndogo

ii. Wana pembe kubwa na ndefu

iii. Hushambuliwa na magonjwa zaidi kuliko Zebu

iv. Hutoa maziwa kidogo hivyo sio wazuri kuwafuga kwa ajili ya maziwa

v. Wanapatikana katika mikoa ya kanda ya ziwa Victoria

4.3.0 Boran

i. Wana umbile kubwa

ii. Wana nundu kubwa

iii. Wana pembe fupi na wengine hawana pembe

iv. Ni ng’ombe wa maziwa na nyama

v. Wana kua haraka kufikia uzito wa kuchinjwa

vi. Nyama yake huweka mafuta kiasi ni laini na yenye ladha

vii. Wana uwezo wa kuzaa ndama kila mwaka

viii. Huzaa ndama wenye uzito mkubwa

ix. Wanahitaji malisho mengi

Boran wanapatikana Kenya na Tanzania katika Ranchi za Taifa mfano Ranchi ya Manyara na kwa baadhi ya wafugaji binafsi.

 

5.0 MIFUMO YA UFUGAJI WA NG'OMBE WA ASILI.

Kuna mifumo mbalimbali ya ufugaji katika uzalishaji wa ng’ombe wa asili.Mifumo hiyo ni:

i. Ufugaji huria

ii. Ufugaji huria uliochanganyika na kilimo

iii. Ufugaji kwenye ranchi

iv. Ufugaji wa kulisha vyakula vya nafaka kwa wingi.

5.1.0 Ufugaji huria

Ufugaji huria ni mfumo wa ufugaji ambapo wafugaji huhamahama ili kutafuta malisho na maji. Wafugaji hawa hutegemea mifugo kwa ajili ya mahitaji yao yote.

5.1.1 Faida za ufugaji huria

i. Ni njia ya kujihami na ukosefu wa maji na malisho hasa wakati wa ukame/kiangazi

ii. Gharama za kuendesha mfumo huu ni ndogo

5.1.2 Hasara za mfumo wa ufugaji huria

i. Mifugohupoteza nguvu nyingi kwa kutembea masafa marefu, na hivyo kuchukua muda mrefu kukua na kufikia uzito wa kuchinjwa

ii. Ni vigumu kupatiwa huduma za kijamii kutokana na wafugaji kuhamahama.

iii. Mfumo huu husababisha uharibifu wa mazingira endapo mifugo itakuwa mingi.

iv. Kupungua kwa aina mbalimbali za nyasi na mimea katika nyanda za malisho.

v. Mfumo huu umekuwa chanzo kikubwa cha migogoro kati ya jamii za wafugaji na wakulima.

vi. Ni rahisi kwa ng’ombe kuibiwa au kupotea.

vii. Ni rahisi mifugo kushambuliwa na wanyama wakali.

5.2.0 Mfumo huria uliochanganyia na kilimo

Huu mfumo wa kukuza ng’ombe wa nyama hapa Tanzania ambapo wafugaji pia ni wakulima wa mazao hasa ya chakula. Ng’ombe huchungwa kwenye maeneo maalumu yaliyotengwa mbali na mashamba ya mazao. Aidha baada ya kuvuna ng’ombe huchungwa kwenye mashamba.  

5.2.1 Faida za mfumo huria uliochanganyia na kilimo

i. Mfugaji huweza kuuza mifugo na kujipatia fedh za chakula iwapo mavuno ya mazao yatakuwa pungufu.

ii. Samadi huweza kuboresha mbuga za malisho na mashamba.

iii. Mifugo pia huweza kufaidika na masalia ya mazao shambani baada ya mavuno.

5.2.2 Hasara za mfumo huria uliochanganyia na kilimo

i. Ni chanzo cha uharibifu wa mazingira

ii. Ni chanzo cha kuenea kwa magonjwa

iii. Ni chanzo cha migogoro kati ya wakulima na wafugaji

 

6.0 UBORESHAJI WA NG'OMBE WA ASILI.

 Ng’ombe bora wa nyama na maziwa wanaweza kupatikana kutokana na kuchagua ng’ombe wenye sifa nzuri kutoka katika kundi alilonalo mfugaji na kuwaruhusu wazaliane ili kuendeleza kizazi.Uboreshaji huu wa ng’ombe wa asili unaweza kufanyika kwa kupandisha majike ya asili.Mfano Zebu na madume ya asili kama Borani au madume yakisasa.

6.10 Uchaguzi wa ng’ombe bora

Mfugaji anashauriwa achague na aruhusu ng’ombe wenye sifa zifuatazo kuzaliana ili hatimaye awe na kundi la wanyama walio bora.

i. Madume yenye maumbile makubwa yenye uwezo wa kupanda majike

ii. Majike yanayozaa ndama mwenye uzito mkubwa kila mwaka.

iii. Majike yenye kutoa maziwa mengi

iv. Majike yasiyopata matatizo wakati wa kuzaa.

6.1.1 Uchaguzi wa majike bora

i. Atokane na koo zenye uwezo wa kutoa maziwa ya kutosha kulisha ndama ili akue haraka

ii. Awe na uwezo mkubwa wa kumlea ndama

iii. Astahimili magonjwa na kumudu hali ya mazingira anakofugwa

iv. Awe na uwezo wa kuzaa kila mwaka

6.1.2 Uchaguzi wa dume bora

i. Anayekuwa haraka

ii. Awe na uwezo wa kustahimili magonjwa na hali ya mazingira ya eneo la kufuga

iii. Awe na umbo halisi la dume bora

iv. Shingo kubwa

v. Kifua kipana

vi. Awe na miguu imara isiyokuwa na matatizo.

vii. Awe na uwezo wa kutambua majike yaliyo kwenye joto,kuyapanda kwa wakati muafaka na kuweka mimba

viii. Awe na utulivu lakini siyo mwenye aibu na mgomvi

ix. Awe na mapumbu yanayolingana

x. Asiwe mgonjwa kama vile magonjwa ya zinaa ili kuepuka maambukizi kwa majike.

Angalizo:

Chagua dume asiye na mahusiano ya karibu na majike ili kupunguza kutokea kwa vilema na Magonjwa ya Kurithi.

 

7.0 UZALISHAJI WA NG'OMBE CHOTARA.

Ng’ombe chotara ni wale waliopatikana kutokana na kuzalisha aina mbili au zaidi za ng’ombe wa kigeni na wa asili. Ng’ombe chotara wana sifa bora mchanganyiko za ng’ombe wa kigeni na wa asili.

7.1.1 Upandishaji

Ni tendo la ng’ombe dume kumpanda ng’ombe jike aliye kwenye joto. Madume na majike huwekwa pamoja katika uwiano unaoshauriwa katika kipindi chote cha mwaka na kwa mtindo huu ndama huzaliwa katika kipindi chote cha mwaka. Upandishaji huu ndio unaotumika zaidi na wafugaji wa ng’ombe wa asili.

Angalizo:

Hakikisha unapandisha ngo’ombe ili kuwezesha ndama wengine kuzaliwa wakati kuna malisho na maji ya kutosha.

7.1.2 Kupandisha kwa wakati/muda maalum

Upandishaji kwa wakati maalumu hutumika pale inapotakiwa ng’ombe wengi wapate mimba na kuzaa kwa wakati mmoja ambapo kuna maji na malisho ya kutosha. Madume kwa kawaida huchanganywa na majike kwa wakati uliopangwa.

7.1.3 Faida

i. Kurahisisha utunzaji wa ndama kwa kuwa na ndama wengi kuzaliwa kwa wakati mmoja badala ya ndama mmoja mmoja au wachache kila wakati.

ii. Kulenga soko la mifugo kwa kuzalisha ndama wengi watakao kuwa tayari kuuzwa kwa wakati mmoja.

iii. Kuoanisha upatikanaji wa malisho mengi na bora zaidi na kuzaliwa kwa ndama ngo’ombe wakipanda malisho bora na ya kutosha watatoa maziwa kwa wingi, ndama watakuwa haraka na mazao yanayokusudiwa yanapatikana mapema

iv. Inasaidia kuwatambua ng’ombe kwenye kundi ambao hawapati mimba

Angalizo:

Umakini unahitajika katika kumwondoa ng’ombe ambaye hajapandwa kwa wakati huo.

 

8.0 UBORESHAJI NA UHIFADHI WA MALISHO ASILIA.

Chakula kikuu cha ng’ombeni nyasi na majani jamii ya mikunde ambayo haia madhara kwaafya ya mnyama.

8.1.0 Malisho ya Asili

Malisho haya kwa kawaida hukua haraka na kupoteza viinilishe muhimu, kwa muda mfupi baada ya mvua. Malisho ya asili huwa na viinilishe vinavyotosheleza mahitaji ya mifugo na wakati wa kiangazi malisho huwa duni na yasiyotosheleza.Wakati malisho yanatosheleza ng’ombe huwa na uzito wa kuridhisha tofauti na wakati wa kiangazi ambapo ng’ombe hupungua uzito. Malisho ya asili ya jamii ya nyasi huwa na upungufu wa viinilishe hususani protini. Mikunde ina tabia yakutopungua viinilishe haraka ikilinganishwa na nyasi.

8.1.1 Malisho yaliyoboreshwa

Malisho ya asili yanaweza kuboreshwa kwa kuongeza mimea aina ya mikunde, kuongeza nyasi bora kwenye malisho, kuongeza samadi kwenye mbuga za malisho. Malisho yaliyoboreshwa yana uwezo wa kuwafanya wanyama wakue haraka na kufikia uzito wa kuchinjwa mapema.

8.1.2 Taratibu za kuboresha malisho/ Mambo ya kuzingatia

i. Uwezo wa kuvumilia hali ya hewa na mazingira yaliyopo

ii. Yawe yenye kuvumilia magonjwa na wadudu waharibifu

iii. Yawe yasiyozidiwa nguvu na magugu

iv. Yawe yenye kustahimili kuchungwa

Inafaa maeneo ya kuchungia/kulishia yatengwe na kugawanywa katika sehemu ambazo nyasi zitaoteshwa na kukuzwa. Hatimaye nyasi hizo zichungwe kwa nyakati tofauti ili

kuepuka uharibifu na kuhakikisha kuwa nyasi zinatosheleza vipindi vyote vya mwaka.Utaratibu huo utasaidia pia kupunguza uwezekano wa mifugo kuambukiza magonjwa.

8.1.3 Uhifadhi wa malisho

Malisho hupatikana kwa wingi wakati wa masika, na wakati huo yana ubora unaotakiwa.Wakati wa masika, mifugo hula malisho na kusaza ambapo wakati wa kiangazi malisho huwa haba na virutubisho hupungua ili kuwa na uhakika na upatikanaji na chakula cha kutosha na bora wakati wote, ni muhimu kuhifadhi malisho ya ziada katika kipindi hicho.

8.1.4 Njia za kuhifadhi malisho

Kuna njia kuu mbili za kuhifadhi malisho nazo ni;

i. Kuyakausha (Hei)

ii. Kuyavundika (Saileji)

8.1.5 Kuyakausha (Hei)

Hei ni majani makavu ambayo yanaweza kulishwa wanyama yangali shambani au kuvunwa na kufungwa kwenye marobota kisha kuhifadhiwa kwa matumizi ya baadaye.

8.1.6 Hatua ya kutayarisha

i. Vuna majani yanapoanza kutoa maua

ii. Yaanike na yageuze majani mara moj au mara mbili kwa siku ili yakauke vizuri

iii. Ukaushaji huchukua siku tatu hadi sita kutegemea aina ya majani au hali ya hewa

iv. Majani yakiisha kauka yafunge kwenye marobota

v. Yahifadhi marobota sehemu isiyoingiza mvua au unyevu

vi. Marobota ya majani makavu yanaweza kutengenezwa kwa mashine au kwa kutumia makasha ya mbao.

vii. Mfugaji mdogo anashauriwa kutumia makasha ya mbao kwa kutengeneza marobota hayo.

viii. Makasha ya mbao yanaweza kutengenezwa kwa kutumia vipimo vifuatavyo,urefu sentimita 75, upana sentimita 45 na kina sentimita 35.

ix. Majani yaliyofungwa katika marobota hutumia sehemu ndogo ya kuhifadhia na pia hupunguza upotevu.

x. Mfugaji anaweza kukadiria kiasi cha malisho atakayotumia kulisha ng’ombe wake kwa msimu wa kiangazi.

8.1.7 Masalia ya mazao shambani

Masalia ya mazao kutoka shambani yanaweza kutumiwa ili kufidia chakula ambacho ng’ombe amekikosa kutokana na uhaba wa majani wakati wa kiangazi. Masalia yanaweza kuwa ya mabua ya nafaka mbalimbali kama vile mahindi, mtama, mpunga, ulezi, ngano au uwele. 

Mengine ni majani ya viazi vitamu, miwa au majani ya jamii ya mikunde kama vile maharage,kunde, njugu mawe au mbaazi.Masalia yanaweza kutumiwa na ng’ombe moja kwa moja bila kuboreshwa. Hata hivyo ng’ombe hawezi kula kwa wingi na hivyo inashauriwa kuyanyunyuzia molasses au magadiili ng’ombe aweze kula mengi zaidi.

8.1.8 Maji

Maji ni muhimu katika kupoza joto la mwili kutengeneza maziwa, kusafirisha virutubisho na kutoa uchafu mwilini kwa njia ya mkojo,kinyesi kupumua na jasho. Ng’ombe akipata maji ya kutosha hukua vizuri, huwa mwenye afya na hutoa maziwa mengi na bora.

Kiasi cha asilimia 85 hadi 87 ya maziwa ni maji. Ng’ombe anapokosa maji hukosa hamu ya kula na hali hiyo ikiendelea hupungukiwa maji na hupoteza uzito. Ng’ombe anaweza kupata maji kwa njia zifuatazo;

i. Kunywa

ii. Kula vyakula vyenye maji maji

8.1.9 Vyakula vya ziada

Hakikisha mifugo yako wanapata vyakula vya ziada kama vile

i. Pumba za mahindi, mtama,ngano

ii. Mashudu ya pamba au alizeti

iii. Madini

iv. Vitamini

8.2.0  UNENEPESHAJI WA NG'OMBE WA ASILI KWAAJILI YA SOKO.

Umri unaofaa kumuuza ng’ombe wa asili ili kupata nyama bora ni miaka mitatu na nusu.Katika umri huu ng’ombe wanaotegemewa kupelekwa kwenye soko kwa ajili ya kuchinjwa ni madume, maksai na mitamba wasiofaa kuzaai. Ili kupata bei nzuri ya ng’ombe mfugaji anatakiwa kuzingatia ubora wa mifugo yake kulingana na madaraja. Hapa nchini ng’ombe wa nyama wanaouzwa wameainishwa katika madaraja matano ambayo ni:

i. Tanzania bora

ii. Daraja la kwanza

iii. Daraja la pili

iv. Daraja la tatu

v. Daraja la nne

9.0 SHUGHULI ZA UTUNZAJI BORA WA NG'OMBE ASALI.

9.1.1 Uogeshaji

Mifugo waogeshwe mara kwa mara ili kuepukana na magonjwa yaenezwayo na kupe pamoja na ndorobo. Uogeshaji unaweza kufanyika kwa kutumia pampu za mgongoni(knapsack sprayers) au kuwatumbukiza katika josho lililotiwa dawa ya kuogeshea.

9.1.2 Kuwapa dawa ya minyoo

Mifugo wapatiwe dawa za minyoo mara kwa mara ili kuhakikisha ukuwaji wao na utoaji wa maziwa uendelee vizuri. Mifugo wapewe dawa za minyoo kila baada ya miezi mitatu

9.1.3 Kuhasi

Ndama dume wasiohitajika kwa ajili ya kuzalisha baadaye wahasiwe kwa njia ya operesheni au kwa kutumia koleo au badizo iwapo ndama ni wakubwa.

9.1.4 Kuwapa ndama alama za utambulisho

Ndama wapewe namba au alama za utambulisho mara wafikiapo miezi 6 tangu kuzaliwa.Utambulisho unaweza kuwa wa chuma au plastiki chenye nambari kwenye sikio,mikato

maalumu katika masikio au chapa katika sehemu malum za mwili.

9.1.5 Kuondoa vichomozo vya pembe

Ndama waondolewe pembe katika mwezi wa kwanza tangu kuzaliwa. Tumia chuma cha moto kuchoma kichomozo chote cha pembe.

10.0 MAZAO YATOKANAYO NA NG'OMBE ASILI.

Kutokana na ufugaji wa ng’ombe wa asili, tunapata mazao yafuatayo:

i. Nyama

ii. Maziwa

iii. Mbolea

iv. Ngozi

v. Kwato

vi. Mifupa

vii. Damu

viii. Pembe

10.1.1 Maziwa

Maziwa yanaweza kusindikwa na kupata mazao mengine ya mifugo kama vile samli, siagina jibini

10.1.2 Pembe na kwato

Mazao haya vile vile yanaweza kutumika kutengeneza gundi, vifungo, mapambo na piavyombo vya kunywea vinywaji mbalimbali na pia kama tarumbeta.

10.1.3 Ngozi

Ni zao linaloweza kutumika katika kutengenezea mikanda, viatu na mikoba ya ngozi.

10.1.4 Damu na Mifupa

Damu na mifupa huweza kutumika kutengenezea vyakula vya kuku na mifugo mingine.Matumizi mengine ya Ng’ombe wa asili:

i. Wanyama kazi

ii. Kutolea mahali

iii. Kipimo cha utajiri

iv. Ajira

v. Kuongeza kipato

vi. Kinga dhidi ya majanga

vii. Kufanyia matambiko .

11.0 DALILI ZA AWALI ZA UTAMBUZI WA AFYA YA NG'OMBE.

 11.1.1 Sifa za mnyama mwenye afya

i. Mchangamfu wakati wote macho maang’avu huku mkia na masikio vikimsaidiakufukuza inzi

ii. Kula na kucheua, kunywa maji vizuri kila siku

iii. Kuonyesha ushirikiano na kutembea pamoja kwenye kundi

iv. Kutembea vizuri

v. Anastuka na kukimbia anapostuliwa na mnyama hatari anapomkaribia kama vile mbwa mwitu, fisi, chui, simba.

vi. Mwili wake una uwezo mkubwa wa kukibadili chakula anachokula kutoa mazao ya kutosha kama vile maziwa.

vii. Anaonekana mwenye nguvu na kwa wale wanaoendelea kukuna wanaongezeka uzito kwa muda mfupi

viii. Kwa mnyama anayekamuliwa mara kwa mara kupiga kelele za kumtafuta mtoto wake,kiwele huwa kimejaa maziwa, chuchu huwa wakati mwingine zimetanuka upande kwa ajili ya kujaa maziwa

ix. Ngozi ya mnyama husisimka mara kwa mara wadudu wapomtambaa

x. Kwa madume, huwa wana hamu ya kuwapanda majike wanaoingia kwenye joto.Miili yao hujengeka vizuri.Korodani hujengeka na kukaa vizuri kwenye nafasi yake(yaani katikati ya miguu)

xi. Pua na midomo huwa na unyevu unyevu wakati wote.

xii. Ngozi kuwa na ulaini unaotakiwa na manyoya hung’aa.

xiii. Kwa kawaida unapo mkaribia mnyama endapo amekaa chini ni lazima atanyanyuka

11.1.2 Dalili za Mnyama anayeumwa

i. Hukosa hamu ya kula na kunywa maji

ii. Mwili kunyong’onyea na kuonekana mchovu

iii. Mnyama kutembea pole pole na kwa taabu na mara nyingi hujitega na wenzake

iv. Pua zake na midomo huonekana kukauka.

v. Kupunguka kwa kiwango cha uzalishaji kama vile maziwa. Kwa madume huduwaa na kuinamisha shingo chini na kukosa hamu ya kuwapanda majike wanaoingia kwenye joto.

11.1.3 Vyanzo vya magonjwa

Magonjwa mengi ya mifugo husambazwa na vijidudu ambao huingia kwenye mfumo wadamu na kusababisha homa na baadae madhara makubwa. Mangonjwa mengi ya mifugo husababishwa na vyanzo kutoka nje ya mwili wa mnyama mfano mazingira machafu anayoishi mnyama, vitu vinavyopelekea vidonda (Vitu vyenye ncha kali) husababisha vidonda ambapo vimelea vinaweza kukaa.Pia mnyama anaweza kupata ugonjwa kutokanana hali za ndani ya mwili kama upungufu wa lishe, mfano: madini, na na magonjwa ya kirithi.Mfano wa wadudu hao ni;

11.1.4 Vimelea (bacteria)

Mfano wa magonjwa yanayosababishwa na bacteria ni chambavu, Blackquarter, Kimeta,Kifua kikuuu, brucellosis (ugonjwa wa kutupa mimba) na ugonjwa wa kiwele.Ng’ombedume huvimba mapumbu.

11.1.5 Virusi (virus) Otatis

Mfano wa magonjwa yanayosababishwa na virusi ni kichaa cha mbwa (Rabies), Ugonjwawa midomo,miguu (foot and mouth disease) na Sotoka (Rinderpest)

11.1.6 Protozoa

Magonjwa yanayo sababishwa na protozoa ni kama ndigana baridi, ndigana kali, ndiganamkojo damu, ndigana maji moyo na nagana.

Angalizo:

Magonjwa yote ya Ndigana husambazwa na makupe, wakati ugonjwa wa naganahusambazwa na ndorobo.

11.1.7 Lishe duni

Upungufu wa viinilishe katika chakula cha mifugo husababisha madhara katika mwili kama ifuatavyo;

i. Husababisha majike kutopata joto mapema

ii. Ndama kuzaliwa na viungo visivyo komaa

iii. Upungufu wa uzalishaji maziwa

iv. Kiwango cha uzalishaji kushuka

11.1.8 Vidonda/michubuko

Kupitia vidonda au michubuko, wadudu wasababishao magomjwa huweza kuingia mwilini kwa mnyama

 11.1.9 Magonjwa ya kurithi

Kama mmoja wa wazazi ana ugonjwa wa kurithi basi kuna uwezekano mkubwa kwa mmoja wa ndama watakaozaliwa kurithi ugonjwa huo.

12.0 MAGONJWA YAENEZWAYO NA KUPE.

12.1.0 Ndigana kali

12.1.1 Dalili zake

i. Homa kali hadi nyuzi joto 42c

ii. Povu kutoka mdomoni na puani

iii. Kuhara choo kilichochanganyikana na kamasi na damu

iv. Tezi kuvimba sana na zenye joto

v. Kuacha kula

vi. Ukungu kwenye macho

vii. Kifo baada ya wiki moja hadi mbili

12.1.2 Tiba

Butalex, Parvexon, tiba iambatane na sindano moja ya kuondoa uvimbe kwenye mapafu kama hali hiyo tayari imeshajitokeza. Tumia Multivitamin ili kuongeza hamu ya kula na Raxis ili kuondoa maji kwenye mapafu.

12.1.3 Kinga/zuia

Zingatia uogeshaji sahihi na Chanjo ya ECF

12.2.0 Ndigana baridi (Anaplasmosis)

12.2.1 Dalili zake

i. Homa hadi nyuzi joto 42C

ii. Kukosa hamu ya chakula

iii. Choo kigumu na makamasi na harufu mbaya

iv. Kifo baada ya siku 8 hadi 10.

12.2.2 Tiba

i. Antibiotic kama vile Oxytetracycline

ii. Imizol.

12.2.3 Kinga

Zingatia uogeshaji sahihi.

12.3.0 Ndigana mkojo damu (Babesiosis) ugonjwa wa kukojoa damu

12.3.1 Dalili zake

i. Mkojo kuwa na rangi ya damu isiyokolea zambarau

ii. Mkojo hutoka kidogo kidogo na kwa muda mrefu

iii. Homa hadi nyuzi joto 40C

iv. Kuacha kula

v. Choo kigumu au kuhara wakati mwingine

vi. Kifo baada ya wiki 1

 

12.3.2 Tiba

Berenil ikisaidiwa na antibiotics za sindano kama vile oxytetracycline (OTC) pia tumia Multivitamin kuongeza hamu ya kula.

12.3.3 Kinga

Zingatia uogeshaji sahihi

12.4.0 Ndigana maji moyo (heart water)

 12.4.1 Dalili zake

i. Kizunguzungu na kuanguka,

ii. Kifo baada ya siku 2

 

12.4.2Tiba

Antibiotics za sindano kama vile oxytetracycline. Kumbuka tiba lazima ifanywe mapema iwezekanavyo

12.4.3 Kinga/kuzuia

Zingatia uogeshaji sahihi

13.0 UTUNZAJI WA KUMBUKUMBU ZA SHAMBA MIFUGO.

Uwekaji wa kumbukumbu ni muhimu sana kwa kila mfugaji. Kumbukumbu zinasaidia katika kujua mambo mengi kama matukio ya magonjwa, tiba, chanjona uogeshaji,gharama za uendeshaji kama gharama za madawa ya tiba, chanjo na uogeshaji, mishahara ya wafanyakazi, faida au hasara baada ya mauzo. Kumbukumbu hizi humsaidia mfugaji kufanya maamuzi katika uendelezaji wa Shamba Lake.

13.1.0 Aina za kumbukumbu

Kumbukumbu muhimu katika ufugaji wa ng’ombe ni pamoja na idadi ya ndama wanaozaliwa, idadi ya ng’ombe, afya ya ng’ombe, kumbukumbu ya mapato na matumizi, ripoti za magonjwa ya mlipuko, vifo Shambani nk.Hata hivyo mfugaji anaweza kuongeza kumbukumbu nyingine kulingana na mahitaji na shughuli zake.

Makala Hii Imeandaliwa na:

Dr. Amani Lugano Mang'alila

Kwa Msaada wa Dr. BUCHEYE,

Toka Kituo cha

Utafiti wa Mifugo (TVLA) West Zone

Tabora -  Tanzania

ushauri maoni       :

  •  +255717274387/+255759417639
  •  Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.

Kuhusu Kangetakilimo

Ni mtandao wa kilimo unaotumia malighafi za kilimo na masoko yaliyopo Tanzania ikiwa imelenga wakulima wadogo wa kati na wakubwa katikata kuwapatia njia bora za kilimo na technologia Kangetakilimo inawawezesha na kuwapa uwezo kwa kutumia technologia katika kilimo kwa mlengo wa kulima kibiashara.  .... Soma Zaidi

 

Download Kangeta Kilimo App

Please publish modules in offcanvas position.