kilimo cha alizeti

kilimo cha alizeti

Alizeti ni zao linalochavushwa kwa upepo au wakala kama nyuki wa asali,vipepeo na wadudu wengine.Bidhaa zitokanazo na alizeti

  • Mafuta; kwa matumizi ya kupika,kula,kutengeneza sabuni na vipodozi
  • Mashudu; lishe ya mifugo kama ngombe wa maziwa,kuku,sungura,nguruwe n.k.
  • Bidhaa shirikishi; asali na nta

MAZINGIRA YANAYOFAA KWA KULIMO CHA ALIZETI

Mwinuko

Alizeti  inaweza kupandwa kwenye maeneo yenye mwinuko kuanzia usawa wa bahari hadi nyanda za juu. Epuka kupanda alizeti maeneo yenye upepo mkali na kwenye kivuli

Udongo

Maeneo yote yenye udongo unaofaa kwa kilimo cha mahindi,mbaazi,kunde,mtama,karanga,choroko,tumbaku na njugu mawe yanafaa kwa kilimo cha alizeti .

MATAYARISHO YA SHAMBA

Shamba la kupanda alizeti ni lazima lilimwe na kusawazishwa vizuri lisiwe na madongo makubwa na hakikisha halituamishi maji kama mbolea ya samadi au ya mifugo inapatikana ni vizuri ikatawanywisha shambani kabla ya kulima.

MBEGU BORA ZA ALIZETI

AGUARA 4

  1. Aina hii ni alizeti chotara.
  2. Inastawi katika mwinuko wa kuanzia ukanda wa chini hadi wa juu.
  3. Inakomaa mapema kwa wastani wa siku102 hadi 109.
  4. Inatoa mavuno ya wastani wa tani 2.7 kwa hekta.
  5.  Ina kiwango cha mafuta cha asilimia 46 cha mafuta.

HYSUN 33

  1. Aina hii ni alizeti chotara.
  2. Inastawi katika mwinuko wa kuanzia ukanda wa chini hadi wa juu.
  3. Inakomaa kwa wastani wa siku 98 hadi106.
  4. Inatoa mavuno ya wastani wa tani 2.5 kwa hekta.
  5. Ina stahimili ugonjwa wa ubwiri unga (powdery mildew).
  6. Ina kiwango kikubwa cha mafuta cha asilimia 41.

NSFH 36

 ·Aina hii ni alizeti chotara.

·Inastawi katika mwinuko wa mita 100 hadi 1,800 kutoka usawa wa bahari.

·Inakomaa mapema kwa wastani wa siku 86 hadi 95.

·Inatoa mavuno ya wastani wa tani 3.4 kwa hekta.

· Ina kiwango kikubwa cha mafuta cha asilimia 40.

·Ina uwezo wa kujikinga na ndege kutokana na tabia ya kichwa chake kuelekeachini (bending characteristics).

NSFH 145

·Aina hii ni alizeti chotara.

·Inastawi katika mwinuko wa mita 100 hadi 1800 kutoka usawa wa bahari.

·Inakomaa mapema kwa wastani wa siku 84 hadi 94.

·Inatoa mavuno ya wastani wa tani 3.6 kwa hekta.

· Ina kiwango kikubwa cha mafuta cha

KUPANDA ALIZETI

Wakati wa kupanda

Alizeti haihitajji mvua nyingi na nizao ninalostahimili ukame 

Hivyo kwa maeneo yenye kipindi kimoja kifupi cha mvua kwa vipindi viwili (December hadi January na Machi hadi Mei ), alizeti ipandwe mwanzoni mwa mwezi Machi.Ni muhimu kuhakikisha kuwa alizeti itavunwa kipindi cha kiangazi kuepuka kuwa na unyevu mwingi

Mbolea ya kupandia

Tumia mbolea ya kupandia aina ya NPK kilo 25 hadi 50 kwa eka. Piga shimo la kupandia lenye kina cha sentimeta 3 hadi 5 kisha tia mbolea kizibo cha maji ya kunywa au kisoda kimoja ndani ya shimo. Rudisha udongo kidogo ndani ya shimo ndipo upande

Umbali wa kupandia

Mbegu ya alizeti ni lazima ipandwe kwenye mistari kwa umbali wa sentimeta 60 kati ya mstari na sentimeta 30 kati ya mimea. Panda mbegu mbili katika kila shimo lililowekewa mbolea ya kupandia. Mbegu hizo mbili zipandwe umbali wa kutosha baina yake ili kuwezesha kuhamishawa au kupunguzwa baadae bila kuathiri mche jirani.

KUPUNGUZA MICHE

Siku 15 baada ya alizeti kupandwa; na endapo mbegu zote mbili zilizopandwa zimeota ni lazima kupunguza miche na kuacha mmea mmoja kila shimo.Mimea ambayo imepunguzwa itumike kujaza mapengo pale ambapo mbegu hata moja haikuota baada ya kujaza mapengo yote,miche ya ziada inaweza kupandwa kwenye eneo dogo jipya, ili kutopoteza miche bila sababu. Eneo kama hilo dogo linaweza kuzalisha mafuta ya kutosha kwa matumizi binafsi ya mkulima nyumbani.

Mbolea ya kukuzia

Siku 30 baada ya kupanda alizeti inahitaji mbolea ya kukuzia. Mbolea inayoshauriwa ni Urea lakini ni bora zaidi kutunia mbolea mseto NPK yenye madini adimu kama Sulfa,Boron,Magnesium n.k. Tia mbolea kuzunguka kila mmea umbali wa sentimeta 5-10 kutoka kwenye shina au katikati ya mistari

PALIZI

Alizeti ni zao lenye wivu na halitaki ushindani na zao lolote jingine.Ni muhimu sana kupalilia alizeti mara kwa mara kuondoa kushindana lishe na unyevu na magugu. Wakati wa palizi ya kwanza ni vizuri kunyanyulia mimea udongo ili kuisaidia kujisimamika vizuri kwa mashina na kupunguza hasara ya kuangushwa mimea kwa upepo

MAGONJWA NA WADUDU WAHARIBIFU

Kama ilivyo kwa mazao yote alizeti pia inashambuliwa na magonjwa na visumbufu vya aina nyingi

MUHIMU

Mkulima anashauriwa kutembelea shamba lake mara kwa mara kukagua na kubaini uwepo wa magonjwa wadudu au visumbufu vingine mapema kabla uharibifu haujawa mkubwa.

Magonjwa

Mgonjwa mengi ya alizeti hasa yale ambayo chanzo ni mbegu au udongo yanadhibitiwa kwa kupanda mbegu bora zenye ukinzani na magonjwa hayo kama Hysun33 na ambazo zimehifadhiwa kwa dawa.Magonjwa muhimu ya alizeti yako kwenye makundi makubwa matatu ; Mnyauko wa uoto;Uoza na unyaufu wa uoto;Ubwiri unga na kutu.

  1. Mnyauko wa uoto.

Mnyauko ni magonjwa yanayosababishwa na fangasi,bacteria na virusi.Mgonjwa mengi ya mnyauko yana chanzo ndani ya udongo au mbegu.Kwa kawaida mnyauko wa fangasi na bacteria hutokea pale ambapo zao limepandwa eneo linalotuamisha maji au kama mbegu zilizopandwa siyo bora.Mbegu bora ina uvumilivu  na ukinzani mkubwa dhidi ya magonjwa ya mnyauko.

Kuepuka magonjwa ya mnyauko inashauriwa kupanda mbegu zilizo bora kuepuka maeneo yanayotuamisha maji na kuzingatia mzunguko wa mazao kwa kuepuka kupanda alizeti kwenye eneo moja mfululizo. Choma masalia yote ya alizeti baada ya kuvuna

                2. Uoza na unyaufu

Uoza na unyaufu wa uoto husababishwa na vimelea hasa fangasi wa makundi mbali mbali. Dalili kuu za magonjwa haya ni kujitokeza kwa madoa madogomadogo rangi ya ugoro au meusi kwenye uoto ambayo baadae huunganika na kuwa uozo au unyaufu wa mabaka makubwa. Endapo dalili hizi zikijitokeza shambani wahi kupiga dawa mapema kuzuia kuenea na kuleta hasara.

Inashauriwa kupiga viuakuvu Super Grino kwa kupishana na Megasin M kila baada ya siku 10 hadi magonjwa yatakapodhibitiwa. Tumia gramu 40 kwenye lita 15 za maji na piga kulowanisha uoto wote.

                3.Ubwiri unga na kuru

Ubwiri unga na kutu ni magonjwa yanayoshambulia uoto na husababishwa na fangasi wanaoshamiri zaidi kipindi cha baridi na unyevu pungufu angani (kipupwe)

Kwa kawaida magonjwa haya hayana madhara kwa zao lililopandwa wakati muafaka kwani hutokea kipindi ambacho alizeti imeshakomaa.Hata hivyo  ubwiri unga na kutu italeta madhara ya uzalishaji mdogokwa alizeti iliyopanmdwa baada ya muda muafaka.

Endapo magonjwa haya yatajitokeza, piga Powershot 250 EC kila baada ya siku 14 hadi 21 kuokoa zao. Tumia Mililita 20 za Powershot kwenye lita 15 za maji na piga kulowanisha uoto wote.

Wadudu na visumbufu

Viwavi,nzi weupe,mchwa na utitiri ni baadhi ya wadudu na visumbufu vinavyoshambulia alizeti.

Endapo uharibifu ni dhahiri na ni mkubwa inashauriwa kupiga Antario kwa kupishanisha na popo au Konto kila baada ya siku 10 hadi 14.

UKOMAVU NA UVUNAJI WA ALIZETI

Alizeti itakuwa imekomaa vichwa vikianza kuwa na rangi njano hadi udongo.Vuna alizeti kwa kukata sahani/vichwa na kuvikausha barabara kabla ya kuhifadhi ni vizuri kuwahi kukamua mafuta mapema kuepuka uharibifu wa zao ghalani.

Kuhusu Kangetakilimo

Ni mtandao wa kilimo unaotumia malighafi za kilimo na masoko yaliyopo Tanzania ikiwa imelenga wakulima wadogo wa kati na wakubwa katikata kuwapatia njia bora za kilimo na technologia Kangetakilimo inawawezesha na kuwapa uwezo kwa kutumia technologia katika kilimo kwa mlengo wa kulima kibiashara.  .... Soma Zaidi

 

Download Kangeta Kilimo App

Please publish modules in offcanvas position.